Tuesday, December 08, 2015

CCM YAIPONGEZA SERIKALI YA AWAMU YA TANO KWA KASI ILIYOANZA NAYO


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM),Ndugu  Abdulrahman O.Kinana(Pichani) akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais,Dkt.John Pombe Magufuli,Makamu wa Rais,Mhe.Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu,Mhe.Kassim Majaliwa kwa kasi nzuri waliyoanza nayo katika utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho.
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akifafanua zaidi jambo mbele ya waandishi wa habari leo Desemba 8, 2015, katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam
 Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiendelea kumsikiliza Ndugu Kinana alipokuwa akizungumza mbele yao mapema leo mchana jijini Dar.
Na Bakari Issa Madjeshi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais,Dkt.John Pombe Magufuli,Makamu wa Rais,Mhe.Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu,Mhe.Kassim Majaliwa Kassim kwa kasi nzuri waliyoanza nayo katika utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho.

Kutokana na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Desemba 07,2015 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM,Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,kikao hicho kilipokea taarifa juu ya utendaji wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Chama,Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu  Abdulrahman O.Kinana amesema Kamati Kuu imeunga mkono hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya  Chama hicho kwa mwaka 2015-2020 inatekelezwa kwa ufanisi.
Pia,Kinana amesema Kamati Kuu ya Chama inapongeza na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kusimamia vyanzo vya mapato ya Serikali ikiwa ni kuhakikisha Mamlaka ya Mapato(TRA) na Mamlaka ya Bandari Nchini(TPA) zinasimamia ukusanyaji wa kodi za Serikali ipasavyo.
Hata hivyo,Ndugu Kinana amesema pamoja na  kuunga mkono na kupongeza kasi waliyoanza nayo,Rais Magufuli,Makamu wa Rais na Waziri Mkuu,Kamati  Kuu inawataka viongozi wengine wote kuiga mfano huu mzuri na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo.

No comments: