Thursday, August 13, 2015

MAALIM SEIF AKUTANA NA VIONGOZI WA CUF – ZANZIBAR


Katibu Mkuu wa
Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na viongozi
wa CUF pamoja na wagombea uwakilishi na ubunge wa Chama hicho Wilaya za Unguja
katika ukumbi wa majid Kiembe Samaki.
Viongozi wa CUF
pamoja na wagombea uwakilishi na ubunge  wakimsikiliza
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati akihutubia kwenye
ukumbi wa Majid Kiembesamaki.
Kaimu Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Ismail Jussa Ladhu, akinukuu baadhi ya vifungu vya
katiba ya chama hicho vilivyoipa uhalali  Kamati tendaji ya chama hicho Taifa kufanya
uteuzi ya wagombea katika majimbo yaliyoongezwa kulingana na hali halisi
ilivyokuwa.
Katibu Mkuu wa
CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi vifaa vya michezo kwa viongozi wa
wilaya na wagombea wa majimbo kama vitendea kazi vya kampeni, ambapo kila jimbo
lilikabidhiwa seti 40 za jezi na mipira 120.
Na Khamis Haji, (OMKR)
Katibu Mkuu wa Chama cha Wanancfhi CUF, Mhe. Maalim Seif
Sharif Hamad amesema upepo wa kisiasa Zanzibar unakivumia vyema chama hicho na matarajio
ni kupata ushindi wa kishindo ambao haujawahi kutokea wa asilimia 80 katika
uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Maalim Seif amesema hayo jana alipokuwa akiwahutubia viongozi
wa Wilaya na majimbo wa chama hicho huko Kiembesamaki, ambapo pia alitangaza
timu itakayo kiongoza chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi mkuu
uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Maalim Seif amesema kwa namna wananchi wanavyokikubali chama
hicho na namna kilivyojipanga na iwapo kila kiongozi na mwanachama atatekeleza
majukumu yake bila ya kulalamika kitachukua idadi kubwa ya majimbo ya uchaguzi
na kushinda nafasi ya Urais kwa kishindo.
“Mazingira yaliyopo Zanzibar ni mazuri sana kwa CUF kupata
ushindi ambao haujawahi kutokea, hivyo kila mmoja wetu aongozwe na dhamira ya
kuchukua nchi mwaka huu, na mara hii haibiwi mtu kura yoyote”, alisema Maalim
Seif.  
Alisema malengo ya CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni
kuwa na idadi ya kutosha ya majimbo yatakayo kiwezesha kufanikisha kikamilifu
mipango yake ya kuwaletea matumaini na maisha bora Wazanzibari chini ya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na wagombea waliopitishwa
na chama kwa upande wa Unguja, Maalim Seif amemtangaza Naibu Katibu Mkuu wa CUF
Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui kuwa ndiye Meneja wa Kampeni za Urais wa Zanzibar,
akisaidiwa na mshauri wake wa Mikakati, Mansour Yussuf Himid.
Aidha kwa upande wa Pemba, Maalim Seif alisema Mratibu wa
kampeni hizo ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi, Hamad Masoud Hamad akisaidiwa
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk.
Maalim Seif alisema Zanzibar hakuna hata jimbo moja ambalo
chama hicho kinaweza kusema kwamba hakina matumaini ya kushinda na kwamba suala
la kushinda au kutoshinda litategemea chama hicho kimejipanga vipi kuchukua
ushindi.
Katibu Mkuu huyo wa CUF ameonya kuwa huu si wakati wa viongozi
na wanachama kuvutana na wala si wakati wa kukumbatia ubinafsi kwa baadhi yao
kupeana majukumu wasiyo yamudu kwa kwa kuzingatia urafiki au ujamaa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu, Ismail Jussa Ladhu alisema CUF
katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu CUF kitakuwa na kampeni ya aina yake kwa
makusudi ya kuwathibitishia Wazanzibari na nchi nzima kuwa kweli kimejiandaa
kuiongoza Zanzibar.
Jussa alisema Agosti 22 wagombea wote waliopitishwa na chama
kugombea Uwakilishi watakwenda kuchukua fomu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa
sherehe kubwa ili kila mtu apate habari kuwa safari ya chama hicho kuiongoza
Zanzibar na kutimiza matarajio yao i imezna rasmi.
“Siku hiyo wagombea wote wa Uwakilishi Zanzibar watakwenda
kuchukua fomu, mwenye kupiga dufu, mwenye kupiga mbwa kachoka, mwenye kupiga
rusha roho ni ruhusa kufanya sherehe hizo”, alisema Jussa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kwa upande wa nafasi ya
Urais wa Zanzibar, ambayo mgombea wake ni Maalim Seif Sharif Hamad atakwenda
kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo Agosti 23, ambapo pia chama hicho
kimeandaa shamra shamra za aina yake.  
Katika mkutano huo, Maalim Seif aliwakabidhi viongozi wa
Wilaya na majimbo seti 40 za jezi kwa kila jimbo moja pamoja na mipira 120. 
Post a Comment