Saturday, October 21, 2006

Dege lililoshusha mitambo ya Richmond

Hapa inaonekana mitambo ikitolewa kupitia mbele ya ndege. Picha hii imepigwa na Mpoki Bukuku maarufu kama Mzee wa Sumo kwa picha zaidi mwaweza kumcheki kwa kubonya hapabaadaye katika mtandao wake)

Haya jenereta hizoo za Richmond hizoooo



Bosi wa Richmond Development Company nchini, Naeem Gire akikagua shehena ya majenereta yaliyowasili nchini leo. (Picha hii imepigwa na Mpoki Bukuku maarufu kama Mzee wa Sumo kwa picha zaidi mwaweza kumcheki kwa kubonya hapabaadaye katika mtandao wake)

Monday, October 16, 2006

Tusipokuwa makini, ipo siku tutaitwa 'Jamhuri ya Mwekezaji'

NASHANGAA kwanini Watanzania sisi, tunaosifika kwa uelewa, wema na uadilifu katika sehemu karibu zote ulimwenguni tunaanza kujidanganya na kisha kujibomoa, tena kwa kasi ya kutisha.
Sisemi kwamba huko nyuma tulikuwa hatujidanyanyi na wala hatudanganywi, la hasha! Nafahamu wazi kwamba yameshawahi kutokea matukio ya kudanganywa na au kudanganya.
Lakini, kama yapo yaliyotokea, yalitokea kwa bahati mbaya sana na yalikuwa yakichukuliwa hatua kali na thabiti sana ili kuyarekebisha na kurudisha mambo katika mstari ulionyooka, na hata sasa naamini hili ntakalolieleza baadaye, haliwezi kuvumiliwa likapita hivi hivi.
Wananchi, wavuja jasho na hata viongozi wao walikuwa na uchungu wa kina na nchi yao hawakupenda kudhulumu, kudhulumiwa, kuiba na au kupora kidogo kilichokuwapo na kisha kujilimbikizia hataka hawakihitaji kwa matumizi ya wakati ule.
Sijui kwa sababu walijengewa misingi ya kuheshimiana, kuthaminiana na kujaliana ambayo kwa sasa imeporomoka kwa kasi hivi karibuni au kwa sababu nyingine pia.
Ninasema hivi kwa uchungu kwa sababu ya matukio kadhaa yaliyowahi kutokea huko nyuma, lakini kubwa likiwa ni hili lililotokea hivi karibuni la kuwapo kampuni ‘hewa’ iliyokaribishwa ili kutukodisha majenereta ya kusaidia kuboresha hali ya uzalishaji umeme.
Taarifa tulizozipata majuzi katika gazeti dada ya hili, The Citizen likinukuu vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, inastusha na inaonyesha kuwa kampuni hiyo, tena kutoka nchi maarufu kama Marekani, haipo katika orodha ya makampuni yanayofanya kazi zake katika Jimbo la Texas.
Na kwamba maelezo ya kampuni hiyo, yanayoonyesha ina makao yake makuu katika Jiji la Houston, jimboni Texas, si ya kweli. Wakati habari hizo zikieleza hivyo, huku kwetu inaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Richmond inaonyeshwa kuwa iliingia mkataba na Serikali ya Tanzania Juni 23, mwaka tulio nao, kwa ajili ya kuikodishia mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi wa megawati 100 ili kuongeza kiasi hicho kwenye gridi ya taifa.
Katika ziara yake katika makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya uzalishaji wa gesi (Songas), Ubungo Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alielezwa kuwa kampuni ya Richmond Development ingeanza kufunga mitambo na kukamilisha baada ya wiki tatu na kwamba umeme wa mitambo hiyo ungeanza kuzalishwa Oktoba 20.
Mradi huo ulikuwa uanze kuzalisha megawati 20 katikati ya mwezi huu na ifikapo Novemba 19, ilitarajiwa kuwa kiasi cha megawati nyingine 80 zingeanza kuzalishwa na kufanya kampuni hiyo izalishe umeme wa dharura wa megawati 100. Kuna maswali mengi ya kujiuliza hapa.
Je, Watanzania, hivi inakuwaje watu tuliowaamini tukawapa madaraka kupitia ofisi za umma ili waweze kutuongoza na kutufanyia masuala yanayohusu maslahi yetu, wakakosa uzalendo namna hii, wakamdanganya hata rais.
Inakuwaje, watu hao wakaweza kula njama na kampuni hewa ambayo tunaambiwa haijasajiliwa wala kutambuliwa si Tanzania tu bali hata Marekani kwenyewe?
Tushukuru Mungu kwamba hawakuwa wamegawiwa kiasi cha mamilioni ya shilingi ya fedha za walipa kodi wanaovuja jasho kutwa kucha katika jamhuri hii ya Watanzania, vinginevyo tungelia na kusaga meno.
Tunafikiri kwamba itakuwa ni jambo la busara kama zitachukuliwa hatua za haraka za kuwawajibisha waliohusika na uzembe huu na kubatilisha mara moja mkataba uliopelekea kampuni hiyo kujipenyeza kijanja nchini mwetu.
Kutokana na mlolongo wa vitendo vinavyofanana na hivi hatuna budi kuwa makini kwa kila tunalolifanya ili kusudi tusije kuangamia na kutumbukia katika matatizo huko mbele ya safari. Nina wasiwasi kweli.
Tusipoangalia na wala kuzingatia na au kuchukulia hatua kali vitendo kama hivi nina hakika kabisa ipo siku tutakuja wananchi wote kuuzwa kwa mwekezaji halafu tutashangaa mikataba iliingiwa nani na kwa maana hiyo hatutakuwa tena na uhuru tutakuwa tukiishi katika nchi ya watu!

Monday, October 09, 2006

Tunaisubiri semina elekezi ya wamachinga


JAMANI ngoja niseme hata kama mpo wale mtakaochukia, lakini huu ndio ukweli. kwamba, haya masuala ya semina elekezi kila sehemu na kila siku, ipo siku wenye pesa zao watalalamikia!
Haiwezekani, muwe mnakula pesa zetu sote nyinyi tuu, kwa kivuli cha semina elekezi au nini, hivi mnaelekezwa nini hicho msichokijua ambacho kinahitaji kuhama mji na kujificha Arusha! Hivi hamuwezi kuelekezwa kwa njia nyingine kuliko hiyo ya kutumia pesa za kodi zetu nyingi tu na tena wengine wametoka Arusha juzi tu, walikuwa na semina elekezi yao wale ni wataalamu wa Wizara ya Afya kutoka kote Tanzania.
Hawa wameingia na hii staili ya kisasa ya kuchapisha fulana kibao na kofia, hivi hizo kofia na mikoba ndivyo vinavyowafanya muelekezwe kwa urahisi au vipi, mbona mawaziri hawakufanya hivyo, na je hamuoni kwamba mnatumia pesa zetu nyingi hivi hivi tu?
Kama lengo ni kutaka tutekeleze ilani ya chama tawala, CCM, basi hata sisi wamachinga tunaisubiri semina yetu, hasa ya jinsi au namna ya kuendesha vibanda na biashara zetu kwa kasi mpya.
Na siyo wamachinga tu hata wafyeka nyasi, wazoa taka, wazibua vyoo, wajenzi, walimu, wauguzi, polisi, wanajeshi, waandishi wa habari n.k, ipo siku nao wanahitaji uelekezi hivi wote hawa wakijichimbia huko tutabaki na nini?
Mimi nilidhani kuwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuwapiga msasa mabosi kama mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya na kisha kutembelea kila wizara na baadaye katika maeneo nyeti hiyo itatosha, lakini inaonekana bado.
Tunasubiri mlolongo wa semina elekezi zaidi ya 20 kama itakwenda kwa mujibu wa wizara zilivyo na kisha nyingine 26 kama itaenda kwa mujibu wa mikoa na baada ya hapo zaidi ya 126 kama itakwenda kiwilaya.
Na kama hiyo itaendelea hivyo, sijui tuna wilaya ngapi na kisha vijiji vingapi na hatimaye mwisho wa siku mwaka 2010 utakuwa umefika kote huko na hakuna kitakachokuwa kimefanyika. Sisemi hivi kwa sababu nina wivu sana. La hasha!
Natambua kwamba Rais Kikwete kwenye semina elekezi ya Ngurdoto alikuwa na maana njema tu ya kutaka watendaji kutekeleza malengo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tunaweza kusema lengo la semina hizi lengo lake kwa tafsiri nyingine ni kutoa elimu kwa viongozi juu ya namna ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete katika semina elekezi alitilia mkazo suala la ubunifu na kuwa na mawazo mapya na kwamba semina elekezi ya Ngurdoto iwe ni hamasa ya kuwapa mwanga wa kubuni miradi yenye kutekelezeka na faida kwa wananchi.
Suala la msingi ambalo pia Rais Kikwete alilisisitiza ni kuwaelekeza viongozi kutumia yote yanayowezekana kuleta mabadiliko ya haraka katika uchumi wa Tanzania.
Semina elekezi, naamini ilikuwa ni ‘shule’ nzuri kwa viongozi kuwapa chagamoto ya kubadilisha hali ya kila Mtanzania kuwa na neema zaidi.
Zamani wakuu wa sehemu mbalimbali walipokuwa wakiteuliwa hawakuwa na fursa ya kuhudhuria semina elekezi kama ya Ngurdoto, kilichokuwa kikifanyika ni kupewa barua ya maelekezo ya kazi na kuanza kazi mara moja. Wengi walishindwa kutofautisha uongozi wao na utekelezaji wa majukumu kwa mihimili mingine ya dola.
Lakini, kikubwa tunachotaka hapa Watanzania ni kuona matunda ya semina hizo kwa viongozi na kwamba kila kiongozi atajitahidi kuwa na miradi ya maendeleo katika eneo lake. Ni vyema msimamo huo wa Rais Kikwete ukachukuliwa kuwa ni changamoto muhimu ili viongozi wote wa Tanzania wawe na aibu kutangaza kwamba maeneo wanayoongoza yamefanikiwa zaidi kimapato wakati wananchi wengi wa eneo hilo wanagubikwa na umasikini.
Hatutarajii semina elekezi ikawa ni kijiwe cha kuvuna posho kubwa kubwa tu na kisha mambo yakabaki vile vile kama ilivyobainika katika baadhi ya maeneo ya nchi alikoweza kutembelea Waziri Mkuu Edward Lowassa. NawatakiaJumapili njema.

Friday, October 06, 2006

Mambo ya mgawo hayo



Mpitanjia akipita kwa uangalifu katika jenmereta zinazofua umemekuingiza katika maduka yaliyopo mtaa wa Mchikichi Kariakoo jijini Dar es salaam, wateja katika maduka hayo wanadai kuna makelele mengi yanayotokana na jenereta hizo. Unapofika katikati ya jiji unaweza kuliita jiji la Dar es Salaam, jiji la makelele kila mtaa ni tak tak tak !!!!

Dar es Salaam angani



Unapokua angani ukikaribia kutua nchi za wanyonyaji unaona kabisa vijimitaa vimejipanga kama ni barabara unaona na hata ukikaa ghorofani unaiona tofauti hiyo angalia hapa katika picha iliyopigwa na Deus Mhagale namna sehemu hii ya jiji inavyoonekana.

Monday, October 02, 2006

Wamachinga



Mfanyabiashara katika mtaa wa Zanaki akiwa kajishika kicha akisikitika baada la tingatinga la jiji kuanza kubomoa kibanda chake saa 8:30 Usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita katika operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara jijini Dar es Salaam. Picha hii ilipigwa na Edwin Mjwahuzi